| ||
| Rais wa TFF, Leodeger Tenga |
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Saalam leo, Rais wa TFF, Leodger Tenga, amesema kuwa sasa uchaguzi huo uliokuwa umepangwa kufanyika Februari 24, hautafanyika tena na hatma yake itategemea ripoti ya tume ya FIFA itakayotua nchini katikati ya mwezi ujao.
Uchaguzi huo ulikuwa umeambatana na malalamiko mengi kutoka kwa baadhi ya wadau wa soka nchini baada ya TFF kupitia kamati yake ya Rufani kuwaengua wagombea kadhaa, wakiwamo Jamal Malinzi aliyekuwa akiwania nafasi ya urais na Michael Wambura aliyetaka kugombea nafasi ya makamu wa rais.
Kutokana na uamuzi wa kamati hiyo inayoongozwa na mwenyekiti wake Iddi Mtiginjola, nafasi ya urais ilibakiwa na mgombea mmoja tu, Athumani Nyamlani, ambaye hivi sasa ndiye Makamu wa Rais wa TFF.
Katika hatua nyingine, Tenga amesema kuwa ushauri alioutoa hivi karibuni kwa kina Malinzi, Wambura na wengine wanaopinga kuenguliwa kwa kuwataka wafuate njia tatu ulitokana na mawazo yake binafsi na wala si vinginevyo.
Tenga alikaririwa akiwaasa kina Malinzi kuwa wanaweza kufuata njia tatu, ambazo ni kwenda kushitaki FIFA, kupeleka shauri hilo kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) au kuomba kamati ya kina Mtiginjola ipitie upya maamuzi yake; mapendekezo ambayo kina Malinzi waliyatekeleza kwa kuomba kamati ipitie upya maamuzi hayo.
Hata hivyo, Mtiginjola alipinga pendekezo la Tenga la kutaka kupitiwa upya kwa maamuzi yaliyowaondoa kina Malinzi kwa kusema wazi kwamba kanuni hazielekezi hivyo na badala yake akawataka wasioridhika na maamuzi ya kamati yake waende kushitaki CAS.
No comments:
Post a Comment